Wednesday, January 16, 2013

FAIDA ZA KARATE

Faida za karate •KUPIGANIA MWENENDO SAHIHI WA TABIA Lengo kuu la karate si ushindi dhidi ya mpinzani au jambo fulani bali ni ushindi dhidi ya nafsi yako mwenyewe. Hii ndio karate-do. Neno ‘do’ lina maana ya ‘njia’. Sote tunajua kwamba hakuna mtu kati yetu aliye mkamilifu hivyo basi ni vema kila mmoja wetu akajitahidi kupunguza madhaifu yake katika safari ya maisha yake. Hii ndio njia ya karate yaani ‘ karate-do’. Madhaifu yanayoelezwa hapa ni kama hasira kali, uzinzi, ulevi, aibu iliyokithiri au kutokujiamini, woga, uvivu, tamaa, husuda, chuki, kujisikia, dharau, majungu n.k. Ni vema ikaeleweka kwamba sanaa haimjengi mtu bali mtu ndiye huijenga sanaa ikiwa na maana ya kuifanya karate kuwa sanaa bora na muhimu katika maisha yetu tofauti kabisa na ambavyo imekuwa ikichukuliwa. Lakini kamwe karate haitoweza kumsaidia mtu kitabia mpaka pale atakapo pata mafunzo kutoka kwa mwalimu ambaye ni msomi na mtaalamu wa sanaa hiyo. Wataalamu na wasomi wa karate wapo wachache mno na walimu wengi si wataalamu hivyo ni vema kuwa makini mara mtu atafutapo shule ya kujifunza kwasababu ni vigumu mno kupima utaalamu na elimu ya mwalimu. •UWEZO WA KUJIHAMI PASIPO KUHITAJI SILAHA Kama ndege, wanyama na mimea mbalimbali ina namna au mbinu za kujihami kwanini asiwe binadamu ?!. Karate inamuwezesha karateka kuweza kujihami katika mazingira hatarishi pasipo kujali umri, jinsia,nguvu au umbo alilonalo. Itagharimu nguvu ndogo sana pamoja na ustadi sahihi wa mbinu ya karate katika kuimudu hali ya hatari. •NIDHAMU NA KUJITAMBUA KATIKA MAZINGIRA MBALIMBALI Karateka ni lazima muda wote awe mwenye nidhamu, aitambue nafsi yake pamoja na mazingira yanayomzunguka. Hii itamuwezesha kutimiza wajibu wake pale atakapo hitajika kufanya hivyo. Lakini pia karateka kama mtu yoyote atakuwa na marafiki wenye tabia mbalimbali hivyo kuna wakati atatakiwa kuheshimu maamuzi na mitazamo yao pindi watakapo kuwa pamoja. Hii kwenye karate tunaita ‘ roho yenye muafaka ‘. •AFYA NJEMA ILIYO IMARA Karate inamsaidia karateka katika kuimarisha afya yake kupitia mazoezi na taratibu mbalimbali zilizopo mafunzoni. Waweza kuitumia karate katika kupunguza uzito wa mwili, kujenga misuli yenye nguvu, kujenga mifupa na viungo imara n.k. •MTU YEYOTE ANAWEZA KUJIFUNZA KARATE Tofauti na sanaa nyingi za mapigano, karate haimbagui mtu katika mafunzo yake. Pasipo kujali jinsia, umri, nguvu au umbo; mtu yeyote anaweza kuanza mafunzo ya karate hata kama ana umri wa miaka hamsini(50) na kuendelea alimradi atakuwa akifundishwa na mwalimu mtaalamu na msomi wa karate ambaye ataweza kutofautisha mafunzo kulingana na umri, jinsia, nguvu na umbo la mwanafunzi.

0 comments:

Post a Comment